KINAYA KAMA NJIA YA KUBAINISHA MAUDHUI: MIFANO KUTOKA RIWAYA YA CHOZI LA HERI NA TAMTHILIA YA KIGOGO
Abstract
Kinaya ni mbinu muhimu ya kimtindo ambayo hutumiwa na waandishi wa riwaya na
watunzi wa tamthilia kuwasilisha ujumbe wao katika kazi za fasihi. Madhumuni ya utafiti
huu yalikuwa: Kuchunguza matumizi ya kinaya kama mbinu ya kimtindo katika
kubainisha maudhui na wahusika katika matini mbili za fasihi ya Kiswahili ambazo ni:
riwaya ya Assumpta K. Matei ya Chozi la Heri na tamthilia ya Kigogo ya Pauline Kea.
Malengo ya utafiti yalikuwa; moja, kubainisha aina mbalimbali za kinaya katika kazi
teule za fasihi; mbili, kueleza jinsi kinaya kimetumika kuendeleza maudhui katika
matini mbili teule za fasihi ya Kiswahili; tatu, kueleza jinsi kinaya kinavyotumika katika
kujenga sifa za wahusika katika kazi teule. Utafiti uliongozwa na Nadharia ya Kimtindo
pamoja na mihimili yake ambayo iliongoza kila sura ya utafiti huu. Nadharia hii inaeleza
kwamba ili kuielewa kazi ya fasihi, msomaji anafaa kuelewa kuhusu mbinu za lugha
ambazo zimetumika. Utafiti huu unaangazia mbinu ya kinaya vile imetumika katika
kubainisha maudhui kama vile uongozi mbaya, ukatili, unafiki na ufisadi. Miongoni
mwa waasisi wake ni Coombes (1953). Riwaya ya Chozi la Heri na tamthilia ya Kigogo
ziliteuliwa kimakusudi kwa msingi wa utajiri wao wa kinaya. Ili kupata data katika
utafiti, mtafiti alisoma vitabu, nadharia, na majarida yanayohusiana na mada ya utafiti.
Utafiti ulitumia muundo wa utafiti wa kimaelezo. Mjadala wa vikundi lengwa uliohusisha
washiriki wanne pamoja na mtafiti ulitumika kukusanya data kutoka katika matini teule.
Data ilichanganuliwa kwa misingi ya malengo ya utafiti. Utafiti unabainisha kuwa kuna
aina mbalimbali za kinaya katika kazi za fasihi. Hizi ni: Hali, drama, mazungumzo,
kilimwengu, na kinaya cha kisokratiki. Utafiti pia unadhihirisha kuwa vinaya vya hali,
mazungumzo na drama ndizo msingi katika ukuzaji wa dhamira na wahusika katika
matini mbili teule. Utafiti huu ulihitimisha kuwa kinaya huwa muhimu katika fasihi
kwa kuwa hutumika katika kubainisha maudhui hasi katika jamiii kwa kuonyesha
matendo maovu ya wahusika wanayotenda kinyume cha matarajio ya wahusika wengine.
Kwa mfano viongozi wanaweza kujitokeza wakitenda matendo hasi kama vile mauaji,
usaliti uzinzi na ubinafsi kinyume na matarajio ya wananchi waliowateua.Tena kinaya ni
muhimu kwa kuwa hutumiwa kueleza sifa za wahusika katika fasihi kwa kuonyesha vile
wahusika wanatenda maovu jambo ambalo ni kinyume cha matarajio ya wahusika
wengine na pia wasomaji.kuwasilisha maudhui na wahusika katika kazi za fasihi na
kinapaswa kufasiriwa kimuktadha ili kuimarisha mawasiliano. Utafiti unapendekeza
kuwa watafiti wa lugha watumie kinaya kama nyenzo ya kuwasilisha masuala
yanayodhihirika katika jamii. Utafiti huu unanuiwa kuwanufaisha watafiti wa fasihi ya
Kiswahili, wanafunzi, waandishi wa riwaya na watunzi wa tamthilia ili kubainisha dhima
ya mitindo ya kifasihi kama vile kinaya katika kuwasilisha ujumbe uliokusudiwa na
mwandishi.